“Hatutaki uchimbaji wa madini na watu wake. Hatumtaki mtoto wake. Hatumtaki bibi yake. Hatuitaki familia yake. Hatuna hamu wala nia ya kuongea nao au kufanya majadiliano na watu wanaohusika na uchimbaji madini. ”
Maneno haya mazito na yenye nguvu yaliongelewa na wawakilishi wawili toka kamati inayoitwa Kamati ya Maafa ya Amadiba (Amadiba Crisis Committee) katika kipindi cha Tatu cha Baraza la Kudumu la Watu wa Afrika Kusini kuhusu Makampuni ya Kimataifa kilichofanyika mwezi Novemba 2018. Kamati ya Maafa ya Amadiba inawakilisha jamii ya Xolobeni, jamii ambayo imekuwa ikipambana kwa miaka kumi na sita kuizuia kampuni kubwa ya uchimbaji wa madini ya Australia inayoitwa Transworld Energy and Minerals (TEM), ili isichimbe ardhi yenye utajiri wa madini ya Titanium katika Pwani ya Msituni ya Afrika Kusini. (1) Kwa mujibu wa Kamati ya Maafa ya Amadiba, ardhi ni sehemu muhimu sana ya utambulisho wa jamii kwa wakati uliopita, uliopo, na wakati ujao. Nonhle Mbuthuma, ambaye ni mmoja kati ya waanzilishi wa kundi hilo anasema, “Tunaamini kwamba tunajitambua kuwa sisi ni akina nani kwa sababu ya ardhi. Tunaamini kuwa mara unapopoteza ardhi, basi unakuwa umeupoteza utambulisho wako.”
Mwezi Aprili 2018, hiyo Kamati ya Maafa ya Amadiba iliipeleka kesi yao katika Mahakama Kuu ya Afrika Kusini ikiwa ni hatua muhimu sana ya kudai haki. (2) Kwa sasa, yaani baada ya miezi kadhaa kupita, na ikiwa ni wiki chache baada ya kipindi cha Baraza la Watu kupita, Mahakama zimeamua kwa kuwapendelea wananchi, zikitangaza kuwa Idara ya Rasilimali za Madini ni lazima ipate ridhaa “kamili na rasmi” toka kwa watu wa jamii ya Xolobeni kabla ya kutoa vibali na haki ya kuchimba madini.
Katika maeneo mbalimbali huko Afrika Kusini na hadi sehemu za mbali, mapambano ya jamii ya Xolobeni yamekuwa ni kesi ya mfano kwa jamii zinazopinga ajenda ya maendeleo inayoburuzwa na sekta ya uziduaji na imeonyesha umuhimu wa mapambano ya kusema HAPANA. Kwa sasa ushindi huu mahsusi umewaamsha na kuwatia motisha wananchi barani Afrika, na ushindi huu umetoa ujumbe na kukumbusha kuwa haki inawezekana kupitia ujenzi wa vuguvugu la mabadiliko na mshikamano ulioandaliwa vizuri na wenye uendelevu.
Ni kutokana na moyo huu wa mshikamano na ujasiri madhubuti katika kuzipinga nguvu za makampuni ndio zilizopelekea kuandaliwa kwa kongamano la tatu la Baraza la Kudumu la Watu wa Afrika Kusini kuhusu Makampuni ya Kimataifa. (3) Kongamano hili lilikuwa ni la tatu na la mwisho katika mchakato wa kusikiliza mashauri ambapo wanajamii waliwasilisha kesi zao dhidi ya makampuni ya kimataifa, huku wakionyesha bayana juu ya ukiukwaji wa haki zao za kibinadamu na haki nyingine; pia walielezea juu ya unyonyaji na uharibifu wa maeneo yao usio na uangalizi maalum. Makampuni haya kwa ushirikiano na Serikali na Mashirika ya Kimataifa ya Fedha kama vile Benki ya Dunia, yamekuwa yakiiendeleza ajenda hii yenye uharibifu ya tasnia ya uziduaji (uchimbaji madini) inayotoa kipaumbele katika kupata faida kuliko watu na sayari yetu—hufanya hayo yote kwa kisingizio cha neno mashuhuri “maendeleo.”
“Tumeadhibiwa sana na vitendo vya kikatili vya uziduaji, kuporwa, kuhamishwa makazi na ukatili mwingi unaofanywa na makampuni ya kimataifa katika harakati zao za kutafuta faida,” hayo ni maneno yaliyosomwa na Mzee wa Baraza wakati akitoa maelezo ya kufunga siku tatu za baraza hilo. “Mambo haya yote yamekuwa yakifanywa mara kwa mara kwa njama zinazofanywa na Serikali na watendaji wake na baadhi ya mashirika katika kuwanyamazisha na katika mazingira fulani hata mauaji ya wananchi. ”
Katika kipindi chote cha mchakato wa baraza hilo, wananchi walitoa na kuelezea kesi ishirini dhidi ya Makampuni ya Kimataifa katika nchi za Madagasca, Malawi, Mauritania, Msumbiji, Afrika Kusini, Swaziland, Tanzania, Zambia na Zimbabwe. Kesi hizi zinahusisha makampuni ya uchimbaji madini na ujenzi wa mabwawa makubwa ya umeme, kilimo-biashara kikubwa, na uporaji wa ardhi – na kila kesi mojawapo inaelezea bayana juu ya njama zilizopo kati ya makampuni, serikali na taasisi za kifedha zinazochangia mfumo wa dunia wa ukandamizaji pasipo kuwa na hofu ya kuadhibiwa. (Soma kuhusu hizo kesi hapa)
Mapambano Kuzuia Mabwawa Makubwa ya Umeme: Zuia Inga 3!
Moja kati ya kesi iliyowasilishwa katika Baraza ni ile ambayo wananchi walikuwa wakipinga ujenzi wa bwawa kubwa la kuzalisha umeme linalojulikana kama Inga katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). (4) Huku kukiwa na ahadi iliyo nyuma ya mradi huo, yaani “kutoa nguvu za umeme na kufungua ujenzi wa viwanda katika bara la Afrika” huku lengo lao likiwa ni kuifanya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuwa na umeme na pia kutoa umeme kwa bara zima la Afrika. Hadi sasa Mradi wa Mabwawa ya Kuzalishia Umeme wa Inga katika mabwawa yake ya kuzalishia umeme ya Inga 1 na Inga 2 yameshawafanya wananchi wengi wa DRC kuwa hawana makazi. Ikiwa ujenzi wa bwawa la kuzalishia umeme la Inga 3 utaendelea kama ulivyopangwa, basi ni dhahiri kuwa takribani watu 37,000 au zaidi watakabiliana na adha ya kupoteza makazi na njia zao nyingine za kujikimu kimaisha.
Makampuni ya uchimbaji wa madini yamepata faida sana kutokana na umeme unaozalishwa toka katika mabwawa mawili ya kuzalishia umeme ya Inga, huku wananchi wengi wakiwa hawana umeme wa uhakika. Kwa sasa, asilimia 85% ya wananchi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hawana umeme. (5) Mpango uliozinduliwa hivi karibuni unaojulikana kama Mpango Fungamanishi wa Rasilimali wa Afrika Kusini (Kwa Kiingereza: South Africa’s Integrated Resource Plan) unaendeleza makubalino kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Afrika ya Kusini ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme kufikia kiasi cha megawati 2500MW za umeme ifikapo mwaka 2030. (6) Kwa sasa, watu wanaoathirika moja kwa moja kutokana na mradi huu mkubwa hawatapata faida yoyote ile huku umeme ukipelekwa katika nchi sita ili kuwezesha uchimbaji wa madini na shughuli nyingine za tasnia ya uziduaji nchini Afrika Kusini. “Sisi tunalala katika maeneo yaliyo na mradi wa mabwawa ya umeme wa Inga lakini tunaishi gizani,” maneno hayo yalisemwa na Jane*, ambaye ni mwanamke mwanaharakati kiongozi wa Kikongo aliyeongea wakati wa Baraza la Watu.
Wakati wa Baraza hilo, wanaharakati walisisitiza pia juu ya mzigo ambao wanawake wanaubeba mara kunapokuwepo na miradi mikubwa kama huu wa Inga ambao unatishia maisha ya watu na shughuli zao za kujikimu kimaisha. Mwanamke mmoja mwanaharakati alisema hivi: “Sisi tunategemea kilimo – tutawezaje kupata chakula chetu? Tutafanyaje ili tuweze kuwalisha watoto wetu? Tutaishije kwa ujumla? Sisi, wanawake tunaoishi Inga tunakitegemea sana kilimo – ni kilimo ndicho kinachotuwezesha kuwalisha watoto wetu. Kwa sasa tunaona hali ya ukavu tu kwa sababu ya bwawa lililojengwa. Uwezo wetu wa kuzalisha chakula umepungua sana kwa sababu ya uwepo wa miundo mbinu mingi inayohusiana na hili bwawa. Kuna wakati ili mlazimu mume wangu kusafiri hadi kijiji kingine ili aweze kuwinda mnyama mdogo kwa sababu kijijini kwetu wanyama wameanza kutoweka. Sisi, tunaoishi karibu kabisa na bwawa la umeme hatuna hata huo umeme.”
Wananchi wanaopambana na bwawa la Inga 3 wameshawasiliana na Serikali zinazohusika, na wameandika barua kwenda kwa serikali ya Afrika Kusini. Pia wamezindua kampeni ya Kupinga na Kuzuia Inga 3 (saini tamko la kuwaunga mkono na kuonyesha mshikamano). Wananchi wanadai na wanataka kampuni zinazojihusisha na ujenzi huo za Kichina, Kihispania, na Afrika ya Kusini ziondoke na ziachane na mpango huo; pia wanaitaka Serikali yoyote ile isishiriki katika uendelezaji wa mradi huo. Upinzaji wao unatoa hamasa sana. Wanafanya kazi katika mazingira ya kutishwa sana ilhali wakiendelea kupambana kuidai na kuipata haki yao ya Kusema HAPANA na kuendelea kudai fidia kwa wale ambao walipoteza makazi yao kutokana mabwawa ya umeme ya Inga 1 na 2.
Wananchi kutoka Afrika Kusini wameshaanza kushughulikia madai ya wanajamii wa Inga, wanaona ndio fursa ya wazi kabisa ya kuwa na mkakati wa pamoja na mshikamano ili kuiwajibisha serikali ya Afrika ya Kusini. “Mto Kongo ni mali ya watu lakini watu wameshaporwa mto huo. Wananchi hawakuwahi kushirikishwa wala kuombwa ridhaa yao. Sisi tuliopo hapa Afrika Kusini hatukuwahi kuelezwa kuwa tutapata umeme toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Na hata kama tungepata umeme toka huko, ni hakika tusingeufurahia umeme huo hasa baada ya kuyafahamu maasi, ubabe wa kivita, na uharibifu unaofanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,” kauli hiyo ilitolewa na Caroline Ntaopane toka muungano unaojulikana kama Mtandao wa Afrika wa Wanawake Dhidi ya Uziduaji wenye Uharibifu (Kwa Kiingereza: African Women network against destructive resource extraction -WoMin Alliance).
Baraza la Watu limekuwa ni jukwaa muhimu sana kwa wananchi wa maeneo ya Kusini mwa Afrika kuweza kushirikishana mapambano yao na kujenga mshikamano, kuwasilisha kesi nzito zinazohusu ukiukwaji wa makampuni, na kutoa changamoto kwa mazoea yanayohusisha neno “maendeleo” kwa kuuanika ukatili ulio ndani yake na hali isiyo endelevu. ”
Kwa sasa wananchi hao na wengine wengi, wanafanya kazi kwa pamoja kujenga kampeni inayotoa fursa na Haki ya Kusema Hapana. Kampeni hii ni “uhamasishaji mpana na makutano ya uanaharakati wa kimataifa na mshikamano.” Kampeni hii ina msingi wake katika kanuni inayozingatia Uhuru, na Taarifa za Mapema kabla ya Kutoa Ridhaa (Kwa Kiingereza: Free, Prior and Informed Consent - FPIC) na kampeni hii inajengwa katika nguvu ya kuandaa mavuguvugu ya mabadiliko, umoja, mashirika ya wanawake na mashirika mengine mengi yaliyo katika jamii kama vile ilivyokuwa kwa jamii ya Xolobeni huko Afrika Kusini na huko Inga katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), yaani makundi yote yanayoinuka na kusema HAPANA kwa nguvu za makampuni, njama za serikali, na kwa ajenda ya maendeleo yenye uharibifu inayowaathiri watu na sayari yetu.
Maggie Mapondera
WoMin African Alliance, http://www.womin.org.za/
* Jina la kiongozi mwanaharakati lilibadilishwa kwa sababu za kiusalama
(1) CIDSE, Xolobeni Community and the Struggle for Consent, November 2017, https://www.cidse.org/gender-equality-blog/xolobeni-community-and-the-struggle-for-consent.html
(2) The Guardian, South African community wins court battle over mining rights, November 2018, https://www.theguardian.com/environment/2018/nov/22/south-african-community-wins-court-battle-over-mining-rights
(3) https://www.stopcorporateimpunity.org/permanent-peoples-tribunal-transnational-southern-africa/
(4) Daily Maverick, SA does not need the Grand Inga Project, November 2018, https://www.dailymaverick.co.za/opinionista/2018-11-08-sa-does-not-need-the-grand-inga-project/
(5) No to Inga 3, Yes to accessible energy across Congo, https://stopinga3.org/en/
(6) South African government releases Integrated Resource Plan draft, August 2018, https://africaoilandpower.com/2018/08/28/south-african-government-releases-integrated-resource-plan-draft/