Wanakijiji katika Wilaya ya Port Loko, nchini Sierra Leone wanashangilia. Hii ni baada ya mapambano ya zaidi ya mwongo mmoja dhidi ya kampuni iliyokuwa imepora ardhi yao na kisha kupanda michikichi ya kuzalisha mafuta ya mawese, mahakama imeamua na kuridhia kuwa ardhi hiyo ni lazima irudishwe kwa wananchi. Kwa sasa wanajaribu kufikiria jinsi watakavyoitumia ardhi yao kubwa ambayo imegubikwa na mistari mingi ya michikichi ya mafuta ya mawese.
Sakata hili la wanakijiji wa Port Loko lilianza mwaka 2009, wakati mwanajeshi wa zamani wa kikosi maalum cha Kiingereza alipokwenda Sierra Leone ili kuchukua ardhi kwa ajili ya upandaji wa michikichi ya mafuta ya mawese kwa niaba ya kampuni ya Uingereza yenye kificho na ambayo haikuwa na uzoefu kwenye biashara ya mazao ya kilimo. Ndani ya kipindi cha miaka mitatu, Ndugu Kevin Godlington alipata mikataba ya kumiliki zaidi ya hekta 200,000 za ardhi katika wilaya za Pujehun, Tonkolili na Port Loko. (1) Mara baada ya hapo, mikataba mingi ya ardhi kati ya hiyo iliuzwa kwa mamilioni ya dola kwa makampuni mengine ambayo yalianza kufanya kazi ya kusafisha hizo ardhi na kisha kupanda mashamba makubwa ya michikichi ya mafuta ya mawese. Mkataba wa ardhi katika wilaya ya Port Loko uliuzwa kwa kampuni ya Siva Group, ambayo ni kampuni yenye makao yake nchini Singapore na inayomilikiwa na mfanya biashara bilionea wa Kihindi. (2)
Mikataba aliyoifanya Ndugu Godlington iliandaliwa na kutengenezwa huku ikikiuka misingi na taratibu nyingi za kimataifa zinazohusu ridhaa ya wananchi. Katika mazingira mengi, viongozi wa wananchi walifikiria kuwa wanasaini risiti za zawadi za Krismasi ingawa kiuhalisia walikuwa wanasaini nyaraka zinazoridhia kuitoa ardhi yao kwa hao wageni. (3)
Kijiji cha Mamanka kilichopo katika mamlaka ya Chifu wa Bureh, Wilaya ya Port Loko, ni moja kati ya wananchi waliokuwa wamepoteza ardhi yao kupitia mchakato huu. Mwaka 2009, kampuni ya Godlington iliyokuwa inaitwa Kampuni ya Kilimo ya Siera Leone (Sierra Leone Agriculture Ltd), ilisaini mikataba ya ardhi iliyoipatia kampuni hiyo hekta 6,557 za ardhi yao, huku ikiwaacha wanajamii wakiwa hawana ardhi ya kutosha kwa uzalishaji wa chakula. Mkataba huo ulikuwa ni sehemu ya mkataba mkubwa wa hekta 41,582 uliokuwa ukihusisha vijiji vingine kadhaa katika wilaya hiyo. Baada ya mwaka mmoja, kampuni ya Siva Group ilizinunua hisa za kampuni yenye jina la Kampuni ya Kilimo ya Sierra Leone (Sierra Leone Agriculture Ltd) kwa asilimia 95% huku Ndugu Godlington akibakiza hisa zake kwa asilimia 5%. (4)
Mwezi Agosti 2018, wawakilishi wa mashirika ya GRAIN, WRM na Bread for All tuliongozana na viongozi wa wanajamii katika maeneo yaliyo athiriwa na mashamba ya michikichi ya mawese katika nchi za Africa ya Magharibi na Kati ili kwenda katika kijiji cha Mamanka ikiwa ni sehemu ya warsha (5) iliyokuwa imeandaliwa na mashirika ya Sierra Leone Network on the Right to Food (SiLNoRF) – (Kwa Kiswahili: Mtandao wa Haki ya Chakula wa Sierra Leone )– , na Women’s Action for Human Dignity (WAHD) – (Jitihada za Wanawake kwa Ajiil ya Heshima ya Mwanadamu).
Tulienda kwa hao wanakijiji tukiwa na nakala ya mkataba wa ardhi ambao ulikuwa umesainiwa na kampuni ya Sierra Leone Agriculture Ltd. (6) Tulishangaa sana, maana hii ndio ilikuwa mara ya kwanza kwa wanakijiji kuiona nakala ya mkataba. Wanakijiji waliopoiangalia ile nakala ya mkataba waligundua mara moja kuwa ilikuwa imejaa ulaghai na udanganyifu. Wananchi walitueleza kuwa hakuna hata kiongozi mmoja toka katika jamii yao aliyekuwa ameusaini mkataba ule, na kwamba baadhi ya saini zilikuwa ni za watu ambao hawana ardhi katika eneo lile. Pia wanakijiji walieleza kuwa walilipinga wazo la huo mradi kwa mara ya kwanza lilipowasilishwa kwao, na kwamba walipojaribu kuizuia hiyo kampuni kwa njia za amani ili wasikate miti, kusafisha ardhi na kumiliki ardhi yao walitishwa na kuogopeshwa sana.
Wanakijiji pia walitueleza jinsi kampuni hiyo ilivyokuwa imetoa ahadi nyingi sana kwao, kwa mfano kampuni iliahidi kutoa ajira nzuri na kujenga shule kwa ajili ya watoto, lakini cha ajabu hakuna hata ahadi moja kati ya hizo iliyotekelezwa. Ni watu wachache tu kati yao ndio walioajiriwa na kampuni tangu ilipoanza kufanya shughuli zake, na hadi wakati huo ulikuwa umeshapita mwaka mmoja bila wafanyakazi wake kulipwa mishahara yao. Tulipovitembelea vijiji vingine vya jirani vilivyokuwa vimeathiriwa na mkataba huo wa ardhi, walitupa maelezo yanayofanana kuhusu jinsi kampuni ilivyoshindwa kutekeleza ahadi zake na jinsi ilivyoongeza umaskini na hali ya usalama mbaya wa chakula katika eneo lao.
Hata hivyo, wanawake wa kijiji cha Mamanka walivutiwa sana na habari waliyoisikia kuhusu mikutano ya viongozi wa jamii toka maeneo mbalimbali ya Sierra Leone pamoja na nchi nyingine za Africa zilizoathiriwa na makampuni yanayoendesha mashamba ya michikichi ya mawese iliyofanyika wilayani Port Loko. Walitambua kuwa hawako peke yao katika mateso wanayoyapitia na kwamba hatua zinaweza kuchukuliwa kuidai ardhi yao.
Mwishoni mwa mikutano mingi, wanawake na washiriki wengine toka kijiji cha Mamanka waliazimia kuwa na madai rasmi kwa kampuni: kuwa ardhi yao irudishwe; na kwamba mishahara na kodi ya pango la ardhi ambayo haijalipwa ilipwe; na kwamba mikataba ya ukodishaji wa ardhi ibatilishwe na kufutwa. Mashirika yote 36 yaliyoshiriki katika mkutano yalisaini tamko la pamoja kuunga mkono madai hayo ya wananchi.
Kwa mujibu wa chifu mwanamke wa Kijiji cha Mamanka, Yarbom Kapri Dumbuya (zamani akijulikana kama Mamasu Dumbuya) alieleza kuwa mapambano ya kudai ardhi yao yalizidi na kuimarika baada ya mikutano hii. Alimweleza Aminata Finda Massaquoi wa Redio Culture wakati alipokitembelea kijiji hicho mwezi Novemba 2018 kuwa, "Tulijifunza kutokana na uzoefu tuliousikia toka kwa wanawake wengine katika nchi yetu na ndani ya bara la Africa."
Mapambano yao hatimaye yaliweza kupata uungwaji mkono toka shirika linaloshughulikia haki za kisheria linaloitwa NAMATI. Maofisa wa shirika hilo waliitembea jamii hiyo na wakakubali kuwasaidia kwa msaada wa kisheria ikiwemo uwakilishi wa kisheria ili kuipeleka kampuni hiyo mahakamani. Baada ya kuhudhuria vipindi kadhaa mahakamani, mahakama iliamua na kuipatia haki jamii, na kisha ikatoa amri ya kimahakama kwa kampuni ya Sierra Leone Agriculture Ltd kurudisha ardhi yote kwa vijiji vya wilaya ya Port Loko na kisha kuwalipa fedha dola za kimarekani 250,000 kama kodi ya pango la ardhi iliyokuwa haijalipwa. (7)
Huku wakitokwa na machozi, wanawake wa Mamanka walimweleza Aminata jinsi walivyopata ahueni baada ya kuipata ardhi yao na jinsi walivyofurahia kutembea juu ya ardhi yao pasipo manyanyaso. Waliwashukuru wote waliosimama pamoja nao wakati wa mapambano yao.
Hata hivyo, bado kuna changamoto nyingi ambazo zipo kwa upande wa wanajamii. Kampuni iliwaacha wakiwa na kisima hatarishi ambacho kilikuwa kimekamilika nusu yake tu huku takribani hekta 1,500 ya ardhi yao ikiwa imegubikwa na michikichi ya mawese. Wanakijiji wa Mamanka hawaelewi cha kufanya kwa uhakika kuhusiana na mashamba hayo ya michikichi ya mawese. Wanajiuliza, je waiondoe hiyo michikichi na kisha kupanda mazao ya chakula? Je, waunde ushirika ili waendelee kuzalisha mafuta ya mawese wao wenyewe? Je, kuna namna wanavyoweza kuyaunganisha mambo yote hayo mawili kwa pamoja?
Kampuni moja inayoweza kuwasiliana na wanavijiji wa Port Loko na kujaribu kuwashawishi na kuwalaghai ili wasaini mikataba mipya ni kampuni ya kidachi inayoitwa Natural Habitats (Kwa Kiswahili: Makazi Asilia). Ni kampuni yenye mashamba ya michikichi ya mawese katika nchi hiyo, pia kampuni hiyo imeanzisha utaratibu wa kilimo cha mkataba na wakulima ili waweze kuzalisha mawese asilia yaliyoidhinishwa na kuthibitishwa. Kutokana na utaratibu wa kampuni hii, mara nyingi kampuni hii imetajwa kuwa ni kampuni bora kuliko makampuni makubwa yenye mashamba makubwa. Lakini wanakijiji wa Port Loko wanapaswa kuwa waangalifu na wawe na tahadhari. Ndugu Kevin Godlington, ambaye ndiye mtu aliyesababisha uwepo wa mikataba mibaya ya ardhi miaka kumi iliyopita, ndiye Afisa Mkuu wa Kampuni ya Natural Habitats! (8)
Ushindi wenye ujasiri wa wanakijiji wa Port Loko uliowawezesha kuipata ardhi yao ni kichocheo kwa jamii nyingine zilizoathiriwa na mashamba ya michikichi ya mawese katika nchi mbalimbali barani Afrika na duniani kote, ikiwemo wale wanaokabiliana na uporaji wa ardhi uliofanywa na kampuni ya Siva Group. Kwa sasa mapambano mapya yanaanza kwa wananchi wa Port Loko ili kuhakikisha kuwa hawapotezi umiliki wa ardhi yao kwa mara nyingine tena.
Kwa sehemu makala hii imetumia taarifa toka kwa Aminata Finda Massaquoi kufuatia safari yake aliyoifanya katika kijiji cha Mamanka mwezi Oktoba 2018.
(1) Unaweza kuiangalia baadhi ya mikataba hiyo kwa kufuata kiungo hiki: https://www.farmlandgrab.org/post/view/22876-land-deals-in-sierra-leone-involving-kevin-godlington
(2) GRAIN, "Feeding the one percent," 7 October 2014: https://www.grain.org/e/5048
(3) Caitlin Ryan, "Large-scale land deals in Sierra Leone at the intersection of gender and lineage", Third World Quarterly, Vol. 39, 2018: https://www.tandfonline.com/doi/full/10.1080/01436597.2017.1350099
(4) Mahojiano yaliyofanywa na Joan Baxter na kisha yakawasilishwa kwa GRAIN, 2013
(5) Azimio la Porto Loko: Wanawake wanasema “Tunazitaka Ardhi Zetu Zirudishwe!”, https://www.grain.org/e/5788
(6) Unaweza kuuona mkataba wa ardhi kwa kufuata kiungo hiki: http://farmlandgrab.org/uploads/attachment/Sla_Bkm_1.pdf
(7) Cooper Inveen, "Sierra Leone ruling against palm oil company will empower communities – campaigners," Reuters, 12 November 2018: https://farmlandgrab.org/28563