Kwa mujibu wa ramani na taarifa za karne ya 18, watu wa jamii ya Gamela, kama walivyoitwa na Wareno waliishi katika eneo linaloitwa Maranhão katika mkoa wa Baixo Pindaré —sehemu inayohusisha manispaa za Codó, Monção, Cajari, Viana na Penalva. Bibi yangu alizaliwa na kukulia katika kijiji cha Capibari kilichopo Penalva; na mama yangu alizaliwa manispaa ya Monção, katika eneo linaloitwa Jacareí, na hapo ndipo mahali nilipozaliwa na mimi. Ni eneo kubwa ambalo lilikuwa likimilikiwa na bado linakaliwa na watu wa jamii ya Akroá-Gamela.
Hivi nilivyo ni matokeo ya mchakato huu wa vurugu na ukoloni. Wakati angali bado kijana, bibi yangu alichukuliwa toka kijijini kwao na familia ya wazungu waliokuwa wakiishi mjini. Mama yangu alizaliwa mbali na kijiji chetu. Mimi pia nilizaliwa mbali na kijiji chetu. Kwa kuwa alama za ukoo zipo katika mwili, na pia zipo—hasasaha —katika nafsi, basi uliwadia wakati ambapo nilianza kujiuliza juu ya alama hizi nilizozibeba. Ni kutokana na mchakato huu wa kuutafuta ukweli, mchakato ambao ninapenda kuuita kuzirejea fikra, ndipo nikaamua kuitafuta mizizi ya ukoo ili niweze kuelewa sawasawa juu ya alama nilizonazo katika mwili na katika nafsi yangu. Lakini jambo hili ninalolifanya si langu binafsi, bali ninalifanya kwa ajili ya jamii yangu kwa pamoja. Kwa sasa tunagundua kuwa sisi hatupo peke yetu hapa ulimwenguni, na kwamba alama hizi si alama za mtu binafsi; bali ni alama za watu, zinazofanana na zenye mizizi yenye kina kirefu.
Kwa muda mrefu, bibi yangu na mama yangu waliutumia ukimya kama mbinu ya mkakati wao. Katika mazingira ambapo Serikali ilikuwa imejikita katika kukanusha mambo mengi, basi uamuzi ulikuwa ni kunyamaza kimya. Nilichojifunza leo ni kwamba ukimya ni aina mojawapo ya upinzani. Ni kipindi ambacho tunapaswa kuwa kimya ili tuweze kuendelea kuwepo. Hivyo, ni kinyume na yale ambayo watu wanayasikia, ukimya haumaanishi ni kuidhinisha vurugu zinazofanywa na Serikali. Kwa upande wa watu wetu wa makabila ya kiasili, ukimya ilikuwa ni —kwa ujumla wake—mkakati wa upinzani. Ili kuwa na uelewa na hisia zinazofahamu kuwa ni kwa nini watu fulani wanafanya jambo moja au jingine, basi ni dhahiri kuwa jambo hilo linawezekana pale tu mtu anapozifanyia uchambuzi kumbukumbu za pamoja za watu hao.
Kwa sasa babu zetu wanasema kuwa tupo katika eneo linaloitwa Taquaritiua, eneo ambalo watu wa makabila ya kiasili waliweza kwenda na kuishi. Watu wa makabila ya asili waliweza kufika mahali hapo toka katika misitu ya mvua, hasa kuanzia mwezi wa Agosti. Utaratibu huo uliingiliwa na kuvurugwa. Paliwekwa mkongo wa simu ambao ulianza kuligawa eneo lao. Na hadi kufikia miaka ya 1960 kulijitokeza mchakato uliojaa vurugu wa uporaji wa ardhi uliofahamika kama "grillaje", mchakato huu uligubikwa na nyaraka na vielelezo vilivyo jaa uongo na udanganyifu. Lengo kuu la vurugu hizi zote ilikuwa ni kukanusha kuwa koo za makabila hayo ya kiasili ziliishi katika ardhi hiyo hapo kabla. Uwepo wetu kama binadamu ulikanushwa pia.
Ukanushaji huo ulianza kutengeneza utengano. Watu walitengwa mbali na ardhi yao kikamilifu kwa kuzingatia: watu, misitu, maji, mito, na maeneo matakatifu. Wakati uzio ulipoanza kujengwa, basi watu nao wakaanza kutengana na kupotezana; na kwa sababu hiyo mipaka ikawekwa katikati ya watu na hivyo kuwatenganisha. Kwa sababu hiyo hata mahusiano kati ya watu yaliingiliwa na kuvurugwa. Tunapochukua hatua za kuokoa na kujiunganisha na kumbukumbu za koo zetu kwa pamoja, basi jambo hilo linawezekana ikiwa tu tutajiunganisha na yale maeneo ambayo ndiyo yanayotoa maana na historia ya uwepo wetu. Mambo haya mawili ni muhimu na yana uhusiano wa karibu sana. Kuyarejea maeneo ya ardhi yetu—ikiwemo hata yale ambayo bado yamewekewa uzio—ni muhimu sana kwa kuwa yanaleta maana ya uwepo wetu kama watu. Hivyo kuna umuhimu wa kufanya kazi ya kuzifanyia tathmini kumbukumbu zetu. Ni mchakato ambao unatokea katika moyo. Ikiwa mchakato huo unatokea katika moyo, basi ni kitu kinachowezekana kukiamsha au kukitupilia mbali.
Historia, Eneo na Kuidai Ardhi
Kuna nyaraka zilizojitokeza kuhusu eneo la [ardhi] lilitolewa kama mchango [kwa watu] wakati wa kipindi cha ukoloni mwaka 1759; jambo ambalo linaleta mkanganyiko maana linaonyesha tulipewa kitu ambacho tayari kilikuwa ni mali yetu. Sasa ninaongelea maalum kabisa kuhusu mojawapo ya ardhi hizo: yaani ardhi ya eneo la Taquaritiua ambayo ipo katika manispaa ya Viana. Nyaraka hizo za mwaka 1759 zinaongelea eneo la hekta elfu 14 au elfu 15. Na zilikuwa nyaraka zenye ulinzi mkali.
Mwaka 1969, Sheria ya Ardhi ya Sarney (1) iliifanya ardhi ya umma kuwa huru kwa ajili ya kutwaliwa, na hadi kufikia mwaka 1970s, eneo la Maranhão lilikabiliwa na mchakato uliojaa vurugu uliojulikana kama "grillage" (Yaani: Uporaji wa Ardhi). Katika miaka ya 1970 na 1980, tuliishi chini ya mchakato ambapo lile eneo lililotolewa kama mchango mwaka 1759 liligawanywa na kuwekewa uzio. Matokeo yake ni kuwa hivi sasa 2018, ardhi yote inayotajwa katika nyaraka hizo za tokea karne ya 18 imesajiliwa kwa majina ya watu binafsi katika usajili wa manispaa ya Viana.
Lakini ilipofikia mwishoni mwa miaka ya 1990, vuguvugu la ndani lililojulikana kama "rumo" lilianza katika maeneo yaliyokuwa yameporwa kwa lengo la kujikimu kimaisha. "Rumo" ni pale familia inapokwenda kufanya kazi katika kipande cha [ardhi] katika maeneo ambayo yamekwisha sajiliwa kwa majina ya watu wengine. Ni mchakato wa kizamani wa kudai na kuipata ardhi. Kulikuwa na msukumo mkubwa wa kutaka kuziondoa hizo familia zilizokuwa zikidai ardhi yao kwa nguvu. Hatimaye maamuzi yalifanyika: “Hapana, kuanzia sasa na kuendelea, wavamizi hawataweza kuweka tena vizuizi; kugawa na kuweka mipaka ya vitalu vya ardhi.” Kwa hakika ulikuwa ni upinzani muhimu sana kwa ajili ya uendelevu wa watu, ingawa ilikuwa ni katika eneo dogo la ardhi. Familia nyingine ziliondolewa na hivyo zikaamua kwenda mjini; watu wakatawanyika. Lakini hivi karibuni mchakato wa kudai ardhi umewezekana kwa kuwa kulikuwa na nguvu kubwa iliyosaidia vuguvugu hili.
Mwaka 2015 tuliamua kudai baadhi ya vipande vya ardhi, hasa vipande vya ardhi vilivyokuwa karibu sana na nyumba za makazi kwa lengo la kupata eneo la kulima. Lakini kuna jambo moja katika mchakato huu wa kuipata ardhi ambalo ni la muhimu sana kwetu, ni lile la kuwa na kumbukumbu za eneo: yaani kudai maeneo matakatifu. Hatudai ardhi kwa ajili ya uzalishaji tu. Tunaidai ardhi kwa kuwa ni mahali patakatifu; ni mahali panapotoa maana ya uwepo wetu.
Hivyo ilikuwa ni muhimu sana tulipoamua kujipanga tena na kuuelezea ulimwengu kuwa sisi tunaishi kama watu. Na hili ndo nililokuwa nikilisema pale mwanzo: kuna wakati wa kukaa kimya ili muweze kuishi na kuwepo, na pia kuna wakati wa kuongea ili muweze kuishi na kuendelea kuwepo. Tupo katika wakati ambao ni muhimu sana—na uliokuwa muhimu sana na utakaoendelea kuwa muhimu sana—yaani tuongee ili tuweze kuendelea kuwepo na kuishi.
Mpangilio, Chuki na Vurugu
Tangu mwanzo, tulitaka mpangilio wetu uwe wa kufanya kazi kwa pamoja. Hatukuwa na mtu aliyekuwa ndiye msemaji mkuu: sauti ilipaswa kuwa ya wanajamii wote. Tulipaswa kuanzisha mchakato unaoendelea wa majadiliano miongoni mwetu ili tuweze kufanya maamuzi. Ilikuwa ni mchakato wa kudumu wa kukutana, ili kujenga makubaliano miongoni mwetu; na pia, mchakato ulijengwa katika namna ambayo wazee walitueleza jinsi tulivyokuwa tunajipanga—jambo ambalo kwa wakati fulani lilinyamazishwa ili kutufanya tuendelee kuwepo na kuishi. Lakini jambo hilo halikuwa limepotezwa, na tunaendelea kusema “utaratibu huu umekuwa ndio njia yetu au namna yetu ya kufanya mambo."
Mwaka 2014 tulianza kupata vitisho kutokana na kujipanga kwetu kama watu kwa umoja wetu. Mwaka ule, kampuni ya nishati ya Maranhão, inayoitwa Cemar, ilianza kujenga msongo wa kusafirishia umeme. Tuliwaomba wasimamishe ujenzi ili waweze kukamilisha taratibu na mawakala wa mazingira. Kampuni ya Cemar ilidai kuwa "wanaojiita makabila ya asili" wanazuia maendeleo ya mkoa. Ni dhahiri kuwa watu wengi wanaopinga mradi huu hawawezi kunufaika na hayo maendeleo wanayoyasema; lakini cha ajabu wanaendelea kusema kuwa sisi tunayapinga hayo maendeleo.
Mwezi Aprili 2017, katika majadiliano na radio moja ya wananchi, makamu wa shirikisho anayeitwa Aluísio Mendes alitutaja sisi "tunaojiita makabila ya kiasili,” kuwa ni waandamanaji na wavamizi, na akasema kuwa sisi tunawapora watu wenye nidhamu na watulivu. Waliandaa utaratibu wa "matendo ya amani," lakini kwa sasa tunafahamu kuwa tangu mwanzo, hilo lilikuwa ni tendo la kujiandaa na kulivamia vuguvugu letu la kudai ardhi. Waliendelea na nia yao na wakatuvamia. (2) Ushiriki wa viongozi wa kanisa la Assemblies of God (Kwa Kiswahili: Kusanyiko la Mungu) katika mchakato huu ni jambo jingine muhimu sana. Wao ndio waliokuwa wakisimamia na kupanga mikakati ya upinzani katika mkoa,—na zaidi ya kuandaa na kupanga—walikuwa wakiueneza ujumbe [kuhusu] "wavamizi wanaotishia amani na utulivu." Mambo haya yote yalitoa msingi wa uvamizi. Katika vipindi vya redio watu walieleza kuwa “mashambulizi” tuliyokuwa tukiyafanya yalikuwa yamesababisha baadhi ya watu wazee kufariki na kwamba baadhi ya wanawake mimba zao zilitoka. Maneno hayo yalikuwa ni kama baruti na moto uliowafanya watuvamie. Jambo la kushangaza kabisa, walianza kutulaumu kwa vifo vya watu ambao walikwa hawahusiki na mgogoro na hali iliyokuwepo. Mazingira ya ulipizaji kisasi na chuki yalitengenezwa dhidi yetu.
Jamii Zilizojipanga
Katika Mfumo wa Watu wa Kiasili na Wanajamii wa Maranhão, tayari tunayo makundi mengine ya kiasili kama vile quilombolas, wakazi wa pembezoni mwa mito, makundi ya wavuvi, wakataji wa nazi na wakulima, makundi haya yote yameweza kuwepo kwa uwezeshaji wa vitengo vya serikali. Mfumo huu ulianza mwaka 2011, wakati ambapo vuguvugu linaloitwa Moquibom quilombola lilipoivamia taasisi inayojulikana kwa kifupi kama INCRA (National Institute of Colonization and Agrarian Reform), na hii ilitokana na uwepo kwa vurugu kufuatia kiasi cha wanajamii zaidi ya 400 walipowasilisha madai yao mbele ya shirika hili—huku kukiwa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa (3).
Tarehe 30 Oktoba 2010, kiongozi mmoja wa jamii ya quilombola aliyeitwa Flaviano na aliyekuwa akitokea eneo la Charco aliuawa. Mwendesha Mashtaka wa serikali alitoa maelezo yanayopinga kuhusika kwa wamiliki wa ardhi, wasaidizi wao na walinzi waliokuwa na silaha. Sisi tuliliona jambo hili kuwa ni ujumbe wa wazi kabisa kwa watu wote waliokuwa wakihusika na vuguvugu la quilombola. Mwezi Juni, watu walipiga kambi mbele ya Mahakama Kuu ya Serikali ya Maranhão kwa kuwa ilitolewa amri ya kuwafikisha wamiliki wa ardhi mahakamani kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Flaviano. Baadaye kambi za wananchi zilihamia kwenye makao ya INCRA, kwa kuwa tulifahamu kuwa kitendo cha kupooza kwa mchakato wa uwekaji mipaka ya ardhi ya quilombola kulisababisha vurugu na matishio ya vifo.
Mwaka huo huo, zaidi ya viongozi sabini wa Maranhão walipokea vitisho vya kuuawa. Ilikuwa ni vigumu kutatua shida ya vitisho na vurugu nyingine pasipo kwanza kutatua mgogoro wa ardhi. Hali hiyo ya sintofahamu ilidumu kwa siku kumi na mbili. Tulijikuta tupo pamoja, yaani watu wa quilombola na sisi watu wa jamii za kiasili na watu wa kiasilia na watu wa quilombola; na tukaona kuwa tulikuwa na matatizo yanayofanana: yaani mapambano kwa ajili ya kupata eneo na ardhi yetu kwa mujibu wa fikra za mahali petu tulipotoka. Baadaye kidogo tulifanya juhudi za kumiliki kwa kuweka kambi kwenye majengo maalum, na ilipofikia mwezi Novemba 2013 tulikuwa na kusanyiko jingine katika eneo la Santa Helena, ambapo watu sabini toka watu wa Maranhão na wanajamii wengi wa quilombola walikusanyika. Ndipo tukasema, "tunahitaji kurasimisha muungano na umoja wa pamoja." Ilikuwa ni jambo jema sana, maana tulitumia alama inayo onyesha kuwa fimbo moja ni rahisi kuivunja ilhali fimbo zikiwa nyingi ni vigumu sana kuzivunja. Na hiyo ikabakia kuwa ni alama na ishara ya nia yetu yakuendelea kuungana katika mapambano ya kuipata tena ardhi na maeneo yetu.
Tunahitaji maeneo yetu yaliyo huru. Kwa sababu hii, tunahitaji kuiweka ardhi iwe huru kwa kuondoa vizuizi na uzio uliokuwa umezungushiwa katika ardhi. Lakini kulikuwa na vizuizi vingine vilivyokuwa vikiizuia na kuifunga miili yetu. Tuliamua kuiweka huru ardhi na kuiweka huru miili yetu. Tunautazama mwili kuwa ni kama kifundo cha uhusiano kati yetu na ardhi, maji, mimea, na wadudu. Katika maeneo mengine jambo hili lingehusisha mchakato wa kuuondoa ukoloni. Wakati watu wanapoipata nguvu itokanayo na uwepo wa ardhi yao, basi nguvu hiyo itaifikia mioyo yao na kuwaweka huru.
Mfungamano wetu ni huu mradi wa muungano na umoja miongoni mwetu tunaoendeleza mapambano. Mtazamo wetu hauangalii kile ambacho watu wengine watatufanyia sisi. Kwa hakika si shirika au muungano wa mashirika; na wala si Serikali. Bali ni sisi wenyewe. Ni lazima jambo hili litoke ndani yetu. Na tena, kuzingatia mambo ya msingi ya kumbukumbu ni muhimu sana. Tunapovunja na kukata kata vizuizi na uzio wa waya, tunafanya hivyo kwa sababu vitu hivyo havikuwepo pale hapo kabla; bali kuna siku ndo viliwekwa. Tunapozungumzia kuvunjavunja uzio uliopo ndani yetu, hapo tunazungumzia kuvunja chuki, ubaguzi, vurugu, na mfumo dume. Kutokana na uwezo wetu wa kuweza kujiunganisha na nguvu inayotoka katika ardhi, basi ni lazima tuyaendeleze mapambano yetu.
Na hakuna nafasi ya wazo la mtu mmoja mmoja kumiliki ardhi—iwe ni ardhi kubwa, ya kati, au ndogo, au ndogo zaidi. Mtu hawezi kugawa kundi la mti wa mchikichi (juçaral) vipande vipande (4). Kundi la miti ya mchikichi ni mahali ambapo watu wote wanaweza kwenda kutafuta na kupata chakula. Kimsingi, kuigawa ardhi katika vipande vipande kunaruhusu kuzalisha fikra duni inayofikiria kuwa ardhi ni kama kitu ambacho baadaye unaweza kukiuza. Ardhi si mali yetu. Sisi wanadamu ni mali ya ardhi na dunia. Uwepo wetu unaleta maana kutokana na uhusiano wetu na ardhi.
Hebu tuzungumzie kuhusu mbinu ya Mfumo: Bila shaka si rahisi kuweza kufanya mkutano na meza ili kujadili mambo mbalimbali hata kama meza hiyo ingekuwa ya thamani kiasi gani. Meza inapaswa kuwa ni mahali ambapo watu wanaweza kuongea. Muda wa mazungumzo ni muda ambao kila mtu anahitaji kuongelea kuhusu mapito na uzoefu wake na uwepo wao. Kucheza, kuimba, kupiga ngoma, na kucheza maracas—yote hayo ni sehemu tu ya mambo yatakayounda mazungumzo. Mambo hayo si vitu, bali ni sehemu ya mazungumzo muhimu.
Ikiwa hatuna ukoo wowote ule, basi ni hakika kuwa mapambano yetu yote yataishia kuwa vurugu. Serikali ambayo haiheshimu misingi ya hizi koo ni serikali yenye vurugu na maasi —haijalishi kuwa serikali hiyo ni ya mlengo wa kulia au kushoto. Kanuni hii pia ni muhimu sana kwa vuguvugu lolote lile la mabadiliko bila kujalisha nia yake nzuri: ikiwa vuguvugu la mabadiliko halina msingi katika koo, basi ni hakika vuguvugu hilo litaleta vurugu, kwa kuwa litasababisha fikra ya kuwatenga na kuwakana wengine, na kuwasema kuwa ni wa aina nyingine.
(1) Sheria Nao. 2979 tangu Juni 15, 1969 iliweka na kuifanya ardhi ya umma iweze kuuzwa na ikasababisha uporaji wa ardhi na migogoro ya wakulima. Sheria hii imepewa jina la José Sarney, mmoja kati ya wajumbe wakuu wa serikali wa Maranhão, aliyekuwa gavana wa jimbo wakati huo na baadaye akawa raisi wa Brazili kati ya Aprili 1985 na Machi 1990.
(2) Tarehe 30 Aprili 2017 zaidi ya watu 30 wa makabila ya kiasili walikabiliwa na vurugu kubwa sana kiasi cha kuwaacha watu watano wakiwa wamejeruhiwa kwa risasi (Kum’tum akiwa ni mmoja wao), watu wawili kati yao walipata ulemavu wa mikono (mmoja wao alikatwa kichwa) na wengine kumi na tano walijeruhiwa, wakiwemo vijana wadogo. Kwa taarifa zaidi, tazama hapa: https://www.campoemguerra-reporterbrasil.org/eles-sao-mesmo-indios-a-pergunta-po
(3) Jamii ya Quilombola imeundwa kutokana na koo za watu wa Afrika waliolazimishwa utumwani na serikali ya kibepari ya Brazili. Moquibom ni moja kati ya mashirika ya watu wa jamii ya quilombola wa jimbo la Maranhão, jimbo ambalo ndilo lenye idadi kubwa ya watu wa jamii hii. INCRA ni wakala mwenye dhamana ya kusajili ardhi ya watu wa jamii ya quilombola.
(4) Neno juçaral lina maanisha ni kundi la miti ya michikichi inayotoa chakula kwa ajili ya wanajamii.